Wednesday 6 August 2014

MAMBO YANAYOWEZA KUKUSAIDIA UFANIKIWE KATIKA MAMBO YOTE
Sehemu ya tano
Hebu turudi pale kwenye 3Yoh 1:2, “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote, na kuwa na afya yako; kama vile roho yako ifanikiwavyo.”
Katika neno hili kuna mabo matatu ambayo ni:-
-Kufanikiwa katika mambo yote,
-Kuwa na afya yako,
-Kama vile roho yako ifanikiwavyo.

Sasa ukitaka kuzungumza kwa lugha ya kihesabu, maana hesabu pia ni lugha ya Mbinguni. Na ukitengeneza (algebraic equation) mlinganyo sahili unaweza kufanya hivi:
Let Kufanikiwa katika mambo yote=x
Kuwa na afya yako=y
Roho yako ifanikiwavyo=z

Neno kama linawakilisha alama ya =

Kwa hiyo x+y=Z

Kumbe mafanikio ya mtu yana kanuni za kiroho kama vile lugha ya mbinguni ya hesabu, inavyoeleza hapo juu.


Kwa ujumla kinachozungumziwa hapa ni kwamba, suala la kufanikiwa katika mambo yote na kuwa na afya yako linategemea jinsi gani roho yako inafanikiwa”kama vile roho yako ifanikiwavyo”--yaani kwa kadri roho yako ifanikiwavyo. Roho yako inakuwa ndicho kipimio cha mafanikio na afya yako. Ambayo ni kusema, kufanikiwa rohoni ni kipimio cha mafanikio yako na kufanikiwa rohoni ni kipimio cha afya yako. Kwa hiyo ukitaka kufaniwa katika mambo yako na kuwa na afya, usitafute kufanikiwa, bali tafuta kufanikisha roho yako kwanza. Kwa sababu roho yako ndiyo itakayosema na kupanga ni kwa kiasi gani ufanikiwe na kuwa na afya. Amen!!

Ukifanikiwa kiuchumi/kimwili kabla ya kufanikiwa roho yako, hayo mafanikio yanakuwa mtego kwako na yanakuwa kitanzi. Usipoanza na Yesu, na Yesu asipokuwa mzaliwa wa kwanza wa mafanikio yako ni hatari sana.

Daudi alikuwa ni mtu aliyekuwa amefanikiwa sana maana alikuwa Kiongozi wa juu kabisa katika nchi yake na pia alikuwa na mali nyingi. Hata nchi yote ya Isaraeli ilimtazama yeye. Lakini siku moja alilia kwenye maombi yake kwa Mungu; ukisema “Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu; Unijaribu, uyajue mawazo yangu Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele.”.-Zaburi 139:23-24.

Inawezekana unamiliki kila kitu unachotaka, kwa kiasi ambacho unakula utakacho; wakati wengine wanakula wanachopata. Lakini nikwambie, kama mafanikio yako hayana AMANI na FURAHA, jiulize maswali mawili, matatu. Maana mafanikio ya kila mtu ni lazima yawe na AMANI na FURAHA. Unaweza kuona ni sawa ukioa au kuolewa na huyo mchumba uliye naye sasa. Je! Ni makusudi ya Mungu? Unaweza kuwa na magari na majumba na mali nyingi kama Daudi. Lakini je! Vipi hiyo njia unayoiendea? Yesu amekutangulia? Kama huna uhakika, nakushauri mshirikishe Mungu na kumwambia....Eeee Mungu wangu uliyeziumba mbingu na nchi, umesema utanishauri na kuniongoza njia nitakayo iendea, nakusihi; Ee Mungu, unichunguze, uujue na moyo wangu, unijaribu, uyajue mawazo yangu; Uone kama njia ninayoiendea sasa, italeta majuto ndani yangu katika maisha yangu, Ukanisaidie ee Yesu, na Ukaniongoze katika njia ya milele, itakayonipa AMANI na FURAHA.

Kwa maana tafsiri ya mafanikio ya kiMungu ni lazima yawe na AMANI na FURAHA. Yaani nakuambia ukiwa na AMANI na FURAHA kwanza;...umeshaanza kufanikiwa. Na kama kuna mafanikio ambayo hayaleti AMANI na FURAHA kwenye ndoa yako; basi ni bora yasije. Mafanikio yoyote ambayo yatakuja kuvuruga ndoa yako au mahusiano yako na Mungu; ni bora yaishie hukohuko. Na hii huwezi kujua nini kitatokea mbele yako, ndio maana ni muhimu umpokee Bwana Yesu—yaani uokoke ili yeye akushauri. Yeye ndiye mshauri wa ajabu.
Kwa hiyo mambo yanayofanikisha roho yako, ndiyo pia yakufanya ufanikiwe katika mambo yote; ambayo ni pamoja na:--

  1. Kuokoka
    Kuokoka maana yake ni kumkubali na kumpokea Yesu moyoni mwako, ili awe BWANA na Mwokozi wa maisha yako. Huu ni uhusiano wa mtu mmoja mmoja binafsi, na Mungu wake. Huu sio uhusiano wa familia, au dhehebu au kikundi fulani na Mungu. Kuokoka ni suala la mtu moja binafsi na Mungu wake.
    Mathayo 1:21 inasema; “Naye atamzaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” Malaika wanasema kuwa Yesu atazaliwa ili kuwaokoa watu wake na dhambi zao. Haimaanishi atawaokoa watu; na dhambi ataziokoa...! Hapana. Bali anachomaanisha ni kwamba, atawatenga watu kutoka dhambini. Warumi 10:9-10 na 13, pia inatuambia “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa amaana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa kuwa kila atakaeyeliitia jina la Bwana ataokoka.”
    Mistari hii juu inatueleza lugha ya mahakamani; kwamaba kama mtu hakufanya kosa huwa anaamini hivyo kuwa, kosa hajafanya. Pili anatakiwa kuthibitisha kwa kukiri anachoamini. Akishindwa kuthibitishwa kwa kukiri, huwa anawekwa hatiani kwa kuhukumiwa. Neno linasema unaamini moyoni mwako, basi thibitisha kile unachoamini kwa kukiri. Ndiyo maana kama umeokoka, lakini hukiri hivyo, utashirikishwa mambo mabaya na rafiki zako. Pia utatumwa kununua sigara, pombe, rafiki zako watakutuma uwatongozee, wanaume au wanawake. Maana yake, unahukumiwa kwa sababu hujakiri.
    Ukienda kwenye aina za maneno,Wokovu ni jina au nomino, ambayo kitenzi chake ni kuokoka; na katika hali ya kutendewa tunasema ni kuokolewa.Mathayo 24:13 anatuambia “Atakayevumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokoka”-. Ina maana Wokovu sio jana, bali ni sasa na pia ni suala la kuendelea mpaka mwisho wa maisha yako.
    Mtu yeyote anaweza kuokoka, wengine huwa wanasema..subiri mpaka nikishaoa au kuolewa ndipo niokoke. Wengine huwa wanasema-Mpaka nikiwa mzee na wengine huwa wanafikiri mpaka wakifa ndipo wanaokoka. Mawazo haya sio ya kweli; maana utakuwa unajichelewesha kupata msaada wa Mungu maishani mwako na pia baada ya kufa ni hukumu. Kama wokovu ni baada ya kufa, Yesu asingetufuata duniani. Angesubiri tukishakufa, ndipo atuokoe. Kwa hiyo, kuokoka ni sasa na ni njia ya kufanikisha roho yako na ndiyo inakusaidia kufanikiwa katika mambo yote na kuwa na afya. Amen!!
  2. Kutafakari NENO la Mungu mchana na usiku kutakusaidia ufanikiwe katika mambo yote. Neno sheria maana yake ni NENO la Mungu. Hebu tusome pamoja Zaburi 1:1-3, kwa kuondoa neno “sheri” na kuweka “NENO.” Itasomeka hivi:-,“Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki, wala hausimama katika njia ya wakosaji; wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali NENO la BWANA ndilo limpendezalo, na NENO hilo hulitafakari Mchana na usiku. Naye atauwa kama mti uliopandwa kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, wala jani lake halinyauki; Na kila atendal litafanikiwa.” Hii ni siri, usimwambie mtu. Kutafakari ni kuwaza ulichosoma au kusikia. Maana unapolitafakari NENO, kuna namna fulani ya mabadiliko yanayotokea rohoni mwako na ndiyo yanakufanya ufanikiwe.
    Joshua 1:7-8 inatuambia “...uangalie kutenda sawasawa na (NENO) sheria yote aliyokuamulu...usiiache, kwenda mkono wa kuume au wa kushoto, upate KUFANIKIWA SANA KILA UENDAKO. Kitabu hiki cha torati, kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo UTAKAPOIFANIKISHA NJIA YAKO, kisha ndipo utakapositawi sana.”
    Ukiwa na tabia ya kutafakari neno la Mungu mchana na usiku, utakuwa na si tu kufanikiwa katika mambo yote, lakini pia utakuwa na afya. Kwa nini, ni kwa sababu kutafakari neno, kunafanikisha roho yako kwanza. Katika dunia iliyojaa mabaya, kunenewa vibaya, kutukanwa, kutengwa, kukatishwa tamaa; wewe tafakari NENO la Mungu. Usitafakari hayo mabaya. Unapotafakari Neno, kuna vitu vinatokea, amabavyo ndivyo vinafanya ufanikiwe. NENO linafanya kitu gani kinachofanya ufanikiwe??
    (a) Neno linaponya.
    Zaburi 107:19-20, inatuonyesha jinsi ambavyo unaweza kupitia jangwani katika maisha yako ya wokovu. Yaani unapitia milima-mabonde na unakuwa na dhiki. Lakini 'ukimlilia Bwana katika dhiki zako, atakuponya na shida zako, kwa kulituma NENO lake kukuponya na kukutoa katika mangamizi ya huzuni zote' ili liweze kukujenga kiroho kwa kuleta mabadiliko ya KiMungu na uweze kufanikiwa katika mambo yote na kuwa na afya.
    (b)Neno linakusaidia kusikia malekezo ya Mungu ya jinsi ya hatua za kufuata ili ufanikiwe. Ukitafakari NENO, utaelewa nini unapaswa kufanya na kwa wakati gani; na nini hupaswi. Warumi 10:17
    © Neno linatia nguvu.
    1Wafalme 19:4-8, inatueleza habari za mtu wa Mungu jinsi alivyokuwa amechoka na kukata tamaa kiasi cha kujiombea roho yake afe. Kwa kukata tamaa, kuchoka na kujaa huzuni, akajiinyoosha, akalala chini ya mti unaoitwa mletemu. Akiwa amelala, Malaika akamjia akamgusa, akamwambia; inuka ule. Yule mtu akainuka akala na kunywa, kisha akalala tena. Maana yake alitafakari Neno kidogo, ndiyo maana akalala tena. Ndipo malaika akamgusa mara ya pili, na kumwambia inuka ule!! Maana safari hii ni kubwa mno kwako.
    Kwa nini unakata tamaa mama, baba, kaka, dada? Unarudi nyuma na unalala tu kwa sababu ya huzuni na kukata tamaa. Inuka ule NENO la Mungu, maana ndipo msaada wako ulipo. Kwa nini unakata tamaa na masomo yako, au mahusiano yako, au mpango ulio nao? Wewe tafakari Neno mchana na usiku, maana safari bado ndefu kwako. Kula Neno upate nguvu za kuendelea. Maana, ule mstari wa nane unatuambia; Malaika alimwamsha mara ya pili, ndipo akainuka akala na kunywa, halafu akenda kwa sababu ya nguvu za kile chakula siku arobaini mchana na usiku. Ambayo ina maana, Neno linatia nguvu. Ukitafari Neno unatiwa nguvu, kweli kweli.
    (d)Neno linaweka wazi na kutengaisha roho, nafsi na viungo vya mwili; ili kuiweka huru nafsi iliyosetwa na uweze kueneda kwa roho. Waebrania 4:12,13 inatuambia; “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu, Yesu kuhani Mkuu.” Uwazi huo, unakuwa wa namna ambayo utaweza kutambua mawazo ya Mungu na yasiyo ya Mungu. Ndipo unakuwa na mawazo, nia na hisia ya Kristo ya kukusaidia kufanikiwa katika mambo yote.
    (e)Neno linamsaidia Roho mtakatifu atende kazi kwenye mawazo na mipango yako. Mwanzo 1:1-3 inatuambia “Hapo mwanzo Mungu aliziumba Mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. Mungu akasema, iwe nuru; ikawa nuru.” Kwa nini ROHO alitulia juu ya uso wa maji? Ni kwa sababu kulikuwa hakuna NENO. Mungu alipotamka NENO ndipo Roho akaanza kufanya kazi. Hii ina maana kuwa NENO ndilo linalosaidia Roho mtakatifu afanye kazi kwenye mipango yako. Na ukiwa na Neno, utakuwa na mipango ya kukusaidia ufanikiwe. Na ndipo Roho atakusaidia kuitekeleza mipango hiyo kwa jinsi ilivyo sawasawa.
  3. Maisha ya maombi, yatakusaidia ufanikiwe.
    Kuna tofauti kati ya maombi na maisha ya maombi. Maombi ni kuzungumza na Mungu kwa muda maalum. Lakini maisha ya maombi ni kwenda mbele zaidi ya ratiba uliyojiwekea kwenye maombi yako. Maisha ya maombi ni kuomba muda wowote bila kujali ratiba uliyojiwekea. Usiku au mchana, iwe unatembea au unafanya kazi. Muda wote unakuwa ni wa maombi. Efeso 6:18 inasema hivi:“Kwa sala zote na maombi, mkiali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu kuwaombea watakatifu wote.” Ni muhimu sana maomnbi yawe ni sehemu ya maisha yako-yaani maombi yawe maisha halisi. Maana kuna vita katika ulimwengu wa roho.
    Mtu, familia, eneo au nchi isiyokuwa na maisha ya maombi; hupata hasara kubwa sana. Na kukiwa na waombaji wanaoishi maisha ya maombi, huleta msaada tele. Nchi ya Israel, walichukuliwa kwenda utumwani Babeli. Na Mungu aliahidi kuwa watakaa utumani Babeli, kwa miaka sabini. Sasa wakiwa Babeli, Danieli 9:2-3, inatuambia hivi “Katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la BWANA lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalem, yaani, miaka sabini. Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. ” Muda wa kukaa utumwani Babeli (Iraki ya sasa) kwa miaka sabini, ulikuwa unakwisha. Kwa bahati nzuri, Danieli alikuwa ni mmsomaji wa maandiko na mwenye kuishi maisha ya kuombi. Aligundua kuwa muda wa wao kukaa utumwani kama Mungu alivyokuwa ameahidi, umekwisha na ndipo akamwomba Mungu ali awatoe Babeli na kuwarudisha Israeli.
    Swali la kujiuliza; Kuna haja gani ya Danieli kuomba Mungu awatoe Babeli, ikiwa yeye Mungu ndiye aliyeahidi kwamba, baada ya miaka sabini atawarudisha Yerusalemu???? Je! Bila Danieli kuaomba wasingerudi Yerusalemu?? Maana Kutoka 12:40 inatuambia, “Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana, muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa miaka mia nne na thelathini.” Lakini kumbuka, Mungu hakusema hivyo. Bali alimwambia Ibrahimu“...Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa maka mia nne.”-Mwanzo 15:13
    Sasa miaka 30 iliyozidi, ilitokea wapi? Ni kwa sababu hawakuomba. Wao walijua ahadi ya BWANA inatimizwa bila kuomba. Kumbe maombi ni lazima. Ndio maana Danieli alipoomba, Israeli walipata ukombozi baada ya miaka 70 sawasawa na ahadi ya Bwana. Na Waisreli walipochelewa kuomba, walipata hasara ya adhabu kuongezeka na kuwa miaka 430 badala ya miaka 400. Huwa Machozi yananitoka nikisoma mistari hiyo.
    Wewe je! umejisababishia hasara ngapi kwa kutokuamba? Au umeisababishia familia yako hasraa ngapi kwa kuchelewa kuomba? Taifa lako limepata hasara kiasi gani kwa kuwa wewe hukuomba? Zile ndoto ambazo uliota, halafu hukuzifanyia kazi, zilipotokea na kuwa kweli, ulijisikiaje? Watu wangapi wamekufa kwa uzembe wako wa kunyamaza tu bila kuomba? Ukijibu hayo maswali; ina maanisha, ukiwa na maisha ya maombi, itakusaidia kufanikiwa katika mambo yote na kuwa na afya, maana roho yako inafanikiwa. Bwana Yesu asifiwe sana!
  4. Kumtafuta Mungu kutakusaidia kufanikiwa. Kumtafuta Mungu, maana yake ni kutaka Mungu ajifunue kwenye eneo ambalo unaona msaada wa Mungu hauonekani kwa karibu. Kwa mfano biashara, afya, malezi ya watoto, huduma, kupata mke au mume, kupata visa, kazini n.k Yaani unaweza kuona Mungu akijidhilisha kwa urahisi zaidi kwenye wokovu wako lakini kukawa na ugumu wa Mungu kujifunua kwenye uongozi wako. Ukisoma 2Nyakati 26:3-5 inatuambia kuwa, “Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na miwili...Akafanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyafanya Amazia babaye. Akijitia nia amtafute Mungu katika siku za Zekaria, aliyekuwa na maono ya Mungu; na muda alipomtafuta BWANA, Mungu alimfanikisha.”
    Njia mojawapo ya kumtafuta Mungu ni kwa kufunga. Na kuna aina tatu za kufunga. Kuna kufunga kuutesao mwili, ili mwili utiishwe-Hapa unaweza usile chakula kabisa (Luka 4:2.) Aina ya pili ni kufunga kwa kutokula vyakula fulani tu (Mfano Danieli 10:1-3). Na pia kuna kufunga nafsi-ni kutotazama, kutosikia au kwenda mahali ambapo huwa unapenda kwenda kupiga story (Mfano Zaburi 35:13b, ambayo inasema “Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu.”
    Daudi alikuwa ameomba maombi kuhusu tatizo la mvua. Na alifanya maombi hayo mwaka kwa mwaka, lakini Mungu hakuonekana. Maana yake Mungu hakujifunua na kujidhirisha. “...naye Daudi akautafuta uso wa BWANA...” 2Samueli 21:1. Ukiutafuta uso wa Mungu au ukimtafuta Mungu, basi fahamu ya kuwa Mungu atakusaidia kufanikiwa katika mambo yote.
  5. Jambo lingine litakalokusaidia kufanikiwa katika mambo yote ni Kumjua Mungu. Kumjua Mungu ni kuwa na mahusiano ya karibu sana na Mungu aliyekuokoa. Ayubu 22:21 inatuambia, “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.” Ukijenga mahusiano ya karibu na Mungu awe kama rafiki yako, ni wazi kuwa atakushirikisha siri nyingi sana za maisha yako na ya familia yako. Lakini pia atakushirikisha namna ambavyo unaweza ukafanikiwa katika mambo yote.
    Martha alipomkaribisha Yesu awe Bwana na mwokozi wa maisha yake, akamweka kando, akaendelea kuwa bize na huduma na kazi zake ambazo alijitetea kuwa anamtumikia Yesu. Ni sawa kabisa alikuwa anamtumikia Yesu. Lakini alikuwa bize na huduma kiasi ambacho alisahau kukaa miguuni pa Yesu ili amfundishe, amshauri na kumwongoza njia atakayoiendea. Mwenzake Mariam, aliamua kuketi pamoja na Yesu ili amfundishe jinsi ya kupata mafanikio kwenye huduma yake. Ukiokoka, tafuta mafundisho, penda mafundisho ya kuukulia wokovu-huko ndiko kumjua Mungu. Kinyume na hapo utafanikiwa katika mambo machache tu, na huwezi kufanikiwa katika mambo yote. Usiwe busy kama Martha, bali upende kumjua Yesu kama Mariam. Katika jambo lolote unalolifanya, tafuta kumjua Mungu, ili akuelekeze jambo la kufanya.
  6. Kujazwa na Roho mtakatifu kila siku, ni namna nyingine ya kukusaidia kufanikiwa katika mambo yote. Efeso 5:18 inasema,Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe na roho.Kujazwa na Roho linapokuwa tendo la kila siku, linampa mtu uwezo wa kumshauri na kumwongoza njia atakayoiendea, si katika wokovu tu, bali pia katika kumsaidia kufanikiwa katika mambo yote.
    Kujazwa na Roho kila siku ndiyo ubatizo wa Roho ambao ni Muhimu ufanyike kila siku. Fahamu kwamba:-
    --Kubatiza kwa maji, wamepewa wanadamu -Luka 3:15-17
    --Yesu anabatiza kwa Rho mtakatifu na kwa moto-Luka 3:15-17
    --Yesu hajawahi kubatiza kwa maji isipokuwa wanadamu-Yohana4:1-2
    --Ushuhuda wa Yesu ni mkuu kuliko wa kibinadamu-Yohana 5:34-35
    --Mtu asipokuwa na Roho matakatifu hataurithi uzima-Yohana 3:1-10
    --Mwizi wa msalabani alipata kibali kurithi uzima bila ubatizo wa maji, kwa sababu Yesu alimbatiza kwa Roho na kwa moto-Luka 23:39-43
    --Kosa la baadhi ya watumishi wa Mungu ni kama kosa la Apolo, kuacha kusema kwamba “Yesu ndio njia kweli na uzima” na kusema kuwa “njia ya BWANA ni kwa ubatozo wa Yohana.” Matendo 18:24-28.
    --Roho mtakatifu ndiyo chapa ya Mungu kwa kanisa-1Yohana 5:6-12

Kwa kuwa Roho makatifu ndiye alama ya kanisa kwa kiasi ambacho; kanisa linatambuliwa na Mungu kwa uwepo wa Roho wake; na asiye na Roho, huyo si wake, basi fahamu:-
--Roho mtakatifu ana karama tofautitofauti anazozigawa kadri apendavyo Roho yeye yule-1Wakorintho 12:4-11
--Moja ya karama hizo ni kunena kwa lugha. Na si kila mtu aliyeokoka lazima anene lugha, lakini kunena kwa lugha ni muhimu kwa ajili yako. 1Wakorintho 12:11
--Karama iliyo kuu ni Upendo, ambayo usipokuwa nayo huendi mbinguni, ila usiponena kwa lugha na unao Upendo, unaenda mbinguni. 1Wakorintho 13:1
--Tatizo la baadhi ya watumishi, kwa kutoelewa masuala ya kunena kwa lugha wanazuia watu wasinene kwa lugha-1Wakorintho 14:39.
--Kunena kwa lugha sio lazima kutafsiriwe, kwa kuwa kuna lugha za wanadamu na za mbinguni; amabayo ina maana kuwa, unaweza usielewe kila kitu kinachosemwa wakati wa kunene kwa lugha-1Wakorintho 13:1
--Mara nyingi anayenena kwa lugha, anazungumza na Mungu mambo ya siri baina yao wawili. Kwa hiyo usitake kujua na kufasiri kila kinachonenwa kwa lugha. Mambo mengine ukiyajua unapata shida mwenyewe-1Wakorintho 14:2.

Sasa kunena kwa lugha kuna faida gani haswa???????????????
--Kunena kwa lugha kunaijenga NAFSI ya mtu ambayo iliyobomolewa au kusetwa na uasherati, uzinzi, matambiko, maneno mabaya, kutoa mimba, n.k; ili apate uhuru wa nafsi yako na ndipo unaweza kufanikiwa-1Wakorintho 14:4a
--Pili kunena kwa lugha kunaijega nafsi ili mtu aweze kuishinda huzuni iliyomtawala mtu muda kwa mrefu maishani mwake; na ndipo anaweza kufanikiwa katika mambo yote. Maana mtu mwenye huzuni hafanyi kazi bali anapenda kulala kama Eliya alivyolala chini ya ule mti unaoitwa mletemu-1Wafalme 19:4-8. Pia mtu mwenye mtu mwenye huzuni hawezi kumtumikia Mungu, maana Biblia inatuagiza mtumikieni BWANA kwa furaha”_Zaburi 100:1-2. Sasa ukiwa na huzuni, utumishi wako unakuwa wa taabu sana.

Baada ya mzee yakobo kupata taarifa ya msiba wa mwanae aliyempenda sana, akapatwa na huzuni kuu. Huzuni hiyo ilidumu kwa muda mrefu sana. Mwanzo 37:34-35 inasema kuwa “Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka, wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake akamlilia.” Unaweza kuwa umepitia nyakati mbalimbali ngumu sana kwenye maisha yako.

Nakumbuka baba yangu alifariki nikiwa darasa la kwanza 1992. Tangu wakati huo, nilipopata ugumu kimaisha nilikuwa nalia sana. Na kumwambia Mungu, naomba unisaidie, tazama sina baba; maana kama baba yangu angekuwepo ningekuwa hivi na vile; ningesoma kwa raha. Nakumbuka nilikuwa naweza kulia hata nikiwa njiani nasafiri. Hii ni huzuni inayoweza kumfanya mtu asiwe tayari kupambana na changamoto za kimaisha. Mtu wa huzuni, ana hatari ya kutoa lawama tu kwa matatizo anayoyapitia hata kama angekuwa na uwezo kutatua shida hiyo. Utasikia, kama baba yangu angekuwepo..., kama mama yangu angekuwepo..., kama mwanangu angekuwepo...Hata akiwa na shida ya ndoa yake, utasikia ansema ningelikuwa na baba au mama au kaka!!!!! Sasa kama hujaokoka ni muhimu uokoke ili Mungu akupe namna ya kushinda huzuni. Kwa nini ukae na huzuni miaka miwili, mitatu, minne au mitano wakati upo msaada wa kukusaidia utoke kwenye huzuni?? Kwani ukiendelea kuhuzunika unafikiri utabadilisha kitu gani??? Na kwa nini uhuzunike kiasi hicho kama mtu asiyekuwa na matumaini??? Na kama umeokoka kunena kwa lugha ni moja njia za kukusaidia kushinda huzuni.

Ayubu10:1 inasema, “Nafsi yangu inachoka na maisha yangu; sitajizuia na kuugua kwangu; nitanena kwa uchungu wa roho yangu.” Uchungu ni huzuni iliyozidi kipimo. Huzuni ya muda mrefu inajenga uchungu kwenye nafsi yako. Ilikuwa baada ya kufiwa na watoto wake wote, mifugo yake yote kufa, kuandamwa na magonjwa, pamoja na kutengwa; ndipo Ayubu alipata huzuni na uchungu wa kushiba; kiasi ambacho hakuweza kulia tena; bali alinena kwa lugha. Unaweza kupata mateso kiasi ambacho unayachoka maisha, na kukinai kuishi na kujiombea kufa. Dawa ni kunena kwa lugha mbele za BWANA, maana wakati huo unakuwa huwezi hata kuomba; na ndipo Roho mtakatifu anakuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa, na Roho atazungumza mambo ya siri ya roho yako ili kuijenga nafsi yako. Bwana Yesu asifiwe!!!

1Samueli 1:10-18 inasema “Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe. Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za Bwana, Eli akamwangalia kinywa chake. BASI HANA ALIKUWA AKINENA MOYONI MWAKE; MIDOMO YAKE TU ILIONEKANA KAMA ANENA, SAUTI YAKE ISISIKIWE; KWA HIYO HUYO ELI ALIMDHANIA KUWA AMELEWA. Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako. Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya HUZUNI, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana. Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba. Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena.

Huyu mama alikuwa na huzuni iliyokuwa na mizizi. Huzuni hii ambayo ikatengeneza uchungu ndani yake, ilisababishwa na kunenwa vibaya kwa muda mrefu kwa sababu ya kutokuwa na mtoto. Lakini ashukuriwe Mungu, kwa sababu katika maombi yake Roho mtakatifu alimsaidia KUNENA-ambayo ina maana ni kunena kwa lugha. Ingawa mchungaji wake alimkemea kwa kuwa na dalili ya kulewa. Unaweza kunena kwa lugha na watu wakadhani ya kuwa umelewa. Cha muhimu usiwasikilize; wewe endelea kuimimina roho yako kwa BWANA YESU. Fanya hivyo kila siku na kila saa katika mazingira ya utulivu, na huzuni itakuachilia mara moja, katika jina la Yesu Kristo. Na Mungu wa Israeli akujalie haja ya moyo wako; ili ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako kama vile roho yako ifanikiwavyo. Na roho yako inafanikiwa kwa kunena kwa lugha, kwa kuishi maisha ya maombi, Kumtafuta Mungu, Kumjua Mungu na kutafakari Neno la Mungu mchana na usiku. Jina la BWANA lihimidiwe, tangu leo na hata milele, Katika jina lipitalo majina yote, jina la YESU Kristo, Amen!!!

No comments:

Post a Comment

Welcome